.
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la
Katiba, Mhe. Samuel Sitta amewahakikishia Watu wenye Ulemavu nchini kuwa
wanatendewa haki katika Katiba Mpya itakayopatikana.
Mhe. Sitta ameyasema hayo leo
Septemba Mosi, 2014 katika mkutano wake na baadhi ya viongozi wa
Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) ambalo
lilikuja katika Bunge Maalum kwa lengo la kuwasilisha hoja zenye
msisitizo kuhusu haki za watu wenye ulemavu katika mchakato Katiba Mpya.
Mhe. Sitta amesema kuwa kazi
wanayoifanya ya kuyapokea makundi mbalimbali Bungeni hapo haina lengo la
kuja na hoja mpya na kuziwasilisha katika Bunge hilo, bali ni
mawasiliano ya kawaida yanayohusu safari kutoka Rasimu Mpya ya Katiba
mpaka kufikia katika Katiba Mpya inayopendekezwa ipatikane.
“Jambo lolote lililoandikwa na
binadamu halikosi kasoro, katika Rasimu hii ya Katiba tumegundua
inayomapungufu kadha wa kadha, kuna baadhi ya maoni ambayo
hayakuzingatiwa ndiyo maana tunayafanyia kazi ili yawemo katika Katiba
Mpya itakayopatikana,”.alisema Mhe. Sitta.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Inclusive Development Promoters and Consultants kutoka Dar es
Salaam, Bw. Kaganzi Rutachwamagyo ambaye pia ni mwanachama wa
Shirikisho hilo,amesema kuwa Kikosi cha Ushauri kuhusu masuala ya watu
wenye Ulemavu kimeweka kipaumbele cha msisitizo wao ambao unajielekeza
katika hoja za kuongeza masuala ya mambo ya Muungano ambapo
wamependekeza kuwa kwenye orodha ya Mambo ya Muungano kuongezewe suala
moja zaidi la Nane kwa mujibu wa Rasimu ya Pili ya Katiba ambalo ni
uratibu wa masuala ya haki, usawa na fursa na uwajibikaji kwa watu wenye
ulemavu kama jambo la Muungano.
Bw. Rutachwamagyo ameongeza kuwa
hoja nyingine ya msisitizo inahusiana na suala la uanzishwaji wa chombo
cha uratibu wa haki, usawa wa fursa na uwajibikaji wa haki za watu wenye
ulemavu ambayo hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 33 ya Mkataba wa Kimataifa
wa Haki za Watu wenye Ulemavu na Mkataba mwenza wa nyongeza
iliyoridhiwa kwa pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na amesema
kuwa wanataka chombo hiko kijulikane kama Tume ya Kitaifa Juu ya Haki,
Usawa wa Fursa na Uwajibikaji kwa Watu wenye Ulemavu.
Aidha, Bw. Rutachwamagyo amegusia
pia juu ya hoja nyingine inayohusu suala la Uwakilishi wa watu wenye
ulemavu kwenye Bunge la Tanzania, Baraza la Wawakilishi, Mabaraza ya
Madiwani utamkwe na Katiba na ukokotolewe kwa misingi ya asilimia badala
ya kuweka idadi mahsusi.
“Mathalani, tunapendekeza kifungu
113 kisomeke kuwa asilimia 5% ya Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania watakuwa ni watu wenye ulemavu wakiwakilisha kundi
hili na watapatikana kwa kuchaguliwa na wahusika wenyewe,” alisema .
Aliongeza kuongeza kwa kuzitaja
hoja nyingine ikiwemo suala la matumizi ya lugha sanifu kwa muktadha wa
watu wenye ulemavu na amesema kuwa kuna hali ya matumizi ya misamiati na
islahi ambazo zinakinzana na dhana za walemavu kimataifa hivyo ni vema
kukawa na tafsiri sahihi ya majina kwa watu hao ili kuepuka kukinzana
huko, aidha amegusia pia suala la Hifadhi ya jamii huku akifafanua kuwa
wadau wenye ulemavu nchini wanadai kuwepo kwa ibara maalum ndani ya
Katiba inayoelekeza masharti ya upatikanaji wa hifadhi ya jamii kwa watu
wenye Ulemavu ikiwa ni pamoja na kulipwa gharama ama kupewa unafuu ya
kupunguza makali ya walemavu kwa mujibu wa ibara ya 28 ya Mkataba wa
Haki za Watu wenye Ulemavu ya 2006.
Akiongea kwa niaba ya watu wenye
ulemavu, Mhe. Amon Mpanjo ambaye ni mjumbe wa Bunge hilo amemuomba
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba kuunga mkono sio kupokea maoni
mapya, bali kuyaboresha yale yaliyokwisha wasilishwa hapo awali.
“Tukuombe Mwenyekiti ulisisitizie
Bunge letu Maalum la Katiba liweze kuzingatia haki za watu wenye Ulemavu
ili nao wapate kuwa na maisha bora,” alisema Mpanjo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa
SHIVYAWATA, Bi. Amina Mollel amesisitiza juu ya hitaji la wanawake la
hamsini kwa hamsini na kati ya hizo, asilimia 5% wawe ni wabunge
walemavu na ameitaka Tanzania kuwa mfano wa kuigwa kwa kutoa nafasi
nyingi za uongozi kada mbalimbali kwa walemavu.
“Hii iwe chachu katika kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapewa nafasi kwa uwezo walionao na sio kubaguliwa,” alisema Amina.

No comments:
Post a Comment