Na Magreth Kinabo, Dodoma
Mjumbe wa Bunge Maalum la
Katiba, ambaye pia ni Mwanasiasa mkongwe, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru
ameeleza siri iliyomsukuma kutoa mapendekezo yake ya sura mpya juu ya
lengo la mageuzi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kujitegemea
kuwa ni unyonge wa watu wengi ili waweze kuondokana na umasikini.
Aidha Mzee Kingunge ambaye ni
mjumbe wa Bunge hilo kutoka kundi la 201 alisema alijifunza katika
semina ya Dk. Amos Wako ambaye alikuwa Mwansheria Mkuu wa
Kenya kwamba ili kuweza kuwa na usawa wa binadamu ni lazima kujali
haki za makundi mbalimbali.
Aliyataja baadhi ya makundi hayo, kuwa ni wafugaji, wavuvi, wakulima vijana na mengineyo.
“ Haki zote hizi zilikuwepo
katika Katiba ya mwaka 1977 na Katiba za nchi mbalimbali, lakini
wanaofaidi haki hizo katika nchi hizo ni wale wenye nacho,” alisema
Mzee Kingunge.
Aliongeza kwamba watu wanaishi lakini hawana uhakika wa kuwa na chakula cha kesho.
“ Mimi nimependekeza kwenye
Kamati yangu Namba Nane, mawazo yangu yamepelekwa katika Kamati
mbalimbali na wengine walelezea vizuri kuliko mimi,” alisema.
Mzee Kingunge alisema hayo huku
akitoa mfano wa Hayati wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa
kilichomsukuma kugombania uhuru ni unyonge wa mwafrika, lakini yeye ni
unyonge wa watu wengi.
“Sisi ni waafrika lazima
tujitambue Sisi nani…sisi ni watu kama wengine, wenzetu wa Mashariki
wameendelea kwa sababu ya maarifa ya kisasa ya Sayansi na Teknolojia
na sisi maarifa tunayo na sasa hivi tunaweza kuyapata hata ambayo
hatuna.
“Ninapendekeza jambo kuu moja
kujenga uchumi wa kisasa wa taifalinalojitegemea, maana yake ni tujikite
katika maarifa ya kisasa ya Sayansi na Teknolojia,tufanye mapinduzi
bora ya elimu, kilimo, ufugaji, uvuvi ili yawe ya kisasa,”
alisisitiza.
Alisema pili ni kuanzisha
mchakato wa mapinduzi ya viwanda,ambayo ni kujenga sekta muhimu za
nishati, mawasiliano na miundombinu kwa kuwa yote hayo yanatuelekeza
kwenye kujenga taifa linalojitegemea.
Mzee Kingunge alisema ni vema
kujenga nchi yenye maendeleo linganifu ya kiuchumi na kijamii katika
taifa, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na kijamii, upangaji wa maendeleo
ya kiuchumi na kijamii na kujitegemea, rasilimali za nchi na matumizi
yake na utafiti wa maendeleo
“Katika kujenga dhamira ya
kujenga uchumi wa kisasa wa taifalinalojitegemea, mafanikio katika jambo
yatategemea mambo matatu, ambayo ni wananchi kufanya kazi kwa bidii,
kwa maarifa na nidhamu,” alisema.
Alisema kufanya hivyo ni
kuwaondoa asilimia 65 ya wakulima wanao tumia jembe la mkono, kuhibiti
ufugaji wa kuhamahama na kuhakikisha wana malisho na maji kwa ajili ya
mifugo yao jirani na makazi yao.
Aliwataka wajumbe wa Bunge hilo, walisoma ili waweze kufanya maamuzi ya kihistoria.
Alifafanua kuwa umasikini
hautaondoka kwa miujiza, bali kwa misingi kama hiyo, kwa kuwa haki
nyingine zinategemea uchumi, huki akitoa mfano China waliweza na kuweka
historia.
No comments:
Post a Comment