1. Historia ya Mradi
Mheshimiwa Spika, Katika miaka ya tisini (1990s), Tanzania ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la uhaba wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme, hali iliyopelekea kuwepo kwa upungufu wa umeme na kuathiri shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali ilichukua hatua za dharura za kuanzisha mradi wa kufua umeme wenye uwezo wa kuzalisha Megawati (MW) 100.
2. Upatikanaji wa IPTL
Mheshimiwa Spika, Mwaka 1994 Serikali ilitoa kazi ya uwekezaji kwa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) iliyokuwa inamilikiwa na Kampuni za VIP Engineering and Marketing Ltd ya Tanzania iliyokuwa na Asilimia 30 na MECHMAR Corporation ya Malaysia (MECHMAR) iliyokuwa na Asilimia 70. Kampuni ya IPTL ilipewa leseni ya kujenga, kumiliki na kuendesha (Build-Own-Operate) Mtambo wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa MW 100 kwa kutumia mafuta mazito eneo la Tegeta-Salasala, Dar es Salaam.
Katika Ukurasa wa 52 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC, Kamati imependekeza Mtambo huo utaifishwe.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika, Kulingana na Mkataba wa PPA kati ya TANESCO na IPTL, majukumu ya IPTL yalikuwa ni kujenga, kumiliki na kuendesha (Build, Own and Operate – BOO). Hivyo, kutaifisha Mtambo huo ni kukiuka makubaliano katika Mkataba wa PPA wa tarehe 26 Mei 1995, ukiukwaji wa aina hii ukitokea unaweza kuingiza Serikali katika mgogoro mkubwa ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwenye Mahakama za kibiashara za kimataifa. Aidha utaifishaji wa miradi ya uwekezaji binafsi itakuwa ni njia ya kufukuza wawekezaji binafsi.
|
Mheshimiwa Spika, Tarehe 26 Mei, 1995, TANESCO na IPTL walisaini Mkataba wa PPA kwa muda wa miaka ishirini (20), kwa ajili ya kununua umeme utakaozalishwa na IPTL. Kwa mujibu wa Mkataba huo, IPTL ilitakiwa kuiuzia TANESCO umeme usiopungua Asilimia 85 ya uwezo wa Mtambo (minimum off take). Hata hivyo, uzalishaji wa umeme haukuanza mara moja kutokana na mgogoro uliotokea kati ya TANESCO na IPTL kuhusu gharama halisi za uwekezaji na namna ya kukokotoa Capacity Charges. Hivyo, IPTL ilianza kuzalisha umeme tarehe 15 Januari, 2002. Kutokana na hali hiyo muda wa miaka 20 ya Mkataba ulianza kuhesabiwa tarehe 15 Januari, 2002 baada ya kuanza uzalishaji (Commercial Operation Date).
Mheshimiwa Spika, Pamoja na mambo mengine muhimu yaliyokuwemo katika PPA, Kifungu Na. 6 cha Mkataba huo kinaipa TANESCO wajibu wa kulipa malipo yaliyotajwa hapo juu na kwamba endapo kutakuwa na mgogoro wowote kuhusiana na malipo hayo (Disputed Amount), itafunguliwa Akaunti maalum (Escrow Account) ya kuhifadhi fedha hizo hadi pale pande mbili zitakapokubaliana juu ya uhalali wa malipo yanayobishaniwa. Aidha chini ya PPA, migogoro yote kuhusiana na masuala ya utekelezaji wa Mkataba huo ilitakiwa kuwasilishwa na kuamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) ya London. Hivyo, ilikuwa ni jukumu la kila mhusika katika Mkataba huu kuwasilisha malalamiko yake ICSID yanapotokea.
Katika Ukurasa wa 8 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa mwaka 2004 TANESCO ilifungua shauri la ICSID 2 kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya Capacity Charge.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Taarifa hiyo siyo kweli kwani TANESCO haijawahi kufungua shauri lolote ICSID ya London au Mahakama yo yote dhidi ya Standard Charterd Bank kupinga kiasi kikubwa cha Capacity Charge kama inavyoelezwa katika Taarifa ya PAC. Shauri la ICSID 2 lilifunguliwa tarehe 31 Oktoba 2010 na Standard Chatered Bank Hong Kong (SCBHK) kwa ajili ya kudai malipo ya deni ililonunua kutokana na mkopo uliotolewa na mabenki ya ushirika ya Malaysia kwa IPTL. Wahusika katika Shauri hilo la ICSID 2 ni SCBHK na TANESCO na wala siyo TANESCO na IPTL.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 12 Februari, 2014 ICSID ilitoa uamuzi kuhusiana na Shauri la SCBHK na TANESCO na kuwashauri wakae kukokotoa upya malipo ya Capacity Charge. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kwa pande hizo kutekeleza uamuzi huo kutokana na pande hizo kutokuwa na Mkataba wa kibiashara baina yao. Vile vile, kupitia Shauri la Madai Na. 60/2014, lililofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na IPTL tarehe 4 Aprili, 2014 ilizuia utekelezaji wa maelekezo hayo.
|
3. Mgogoro kati ya IPTL na TANESCO
Mheshimiwa Spika, Migogoro kati ya TANESCO na IPTL ilianza muda mfupi baada ya PPA kusainiwa tarehe 26 Mei 1995. IPTL waliitaka TANESCO wakubaliane bei za kununua umeme kwa kuzingatia gharama za uwekezaji. Pande hizo mbili zilishindwa kukubaliana gharama za Capacity Charge kwa vile TANESCO walidai kuwa gharama zilizoainishwa na IPTL ni kubwa kuliko gharama halisi za uwekezaji. Mwaka 1998, TANESCO iliajiri Kampuni ya Mawakili ya Mkono & Co Advocates kutoa huduma za kisheria kwa kushirikiana na Huntons & Williams ya Marekani. Kutokana na tofauti za gharama za Uwekezaji, Mawakili hawa waliishauri TANESCO ifungue Kesi ICSID nchini Uingereza dhidi ya IPTL ili kupinga gharama hizo.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia ushauri huo wa Mawakili, TANESCO ilifungua Kesi Na.ARB/98/8 ya mwezi Agosti, 1998 ikidai kuwa gharama halisi za uwekezaji ni Dola za Marekani milioni 90 na siyo milioni 163.53 kama ilivyodaiwa na IPTL. Aidha, IPTL ilidai kuwa kiwango cha marejesho ya uwekezaji (Internal Rate of Return-IRR) ni Asilimia 23.10 ambacho pia kilipingwa na TANESCO.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 12 Julai, 2001, ICSID ilitoa uamuzi wa Kesi hiyo pamoja na mambo mengine kwamba:-
i. Gharama halisi za uwekezaji zikiwemo Mtambo na nyumba za wafanyakazi wa IPTL zilizoainishwa katika hesabu ya IPTL zilikuwa ni Dola za Marekani milioni 163.53 lakini ICSID iliona kuwa gharama halisi ni Dola za Marekani milioni 127.20;
ii. Kiwango cha marejesho ya uwekezaji (Internal Rate of Return-IRR) ilikuwa Asilimia 22.31 badala ya Asilimia 23.10 iliyodaiwa na IPTL; na
iii. TANESCO na IPTL wakubaliane mfumo wa malipo ya kununua umeme ukizingatia gharama halisi za uwekezaji na kiwango cha marejesho ya uwekezaji (IRR) cha Asilimia 22.31 kwa kutumia financial modeliliyokubalika na ICSID.
Katika Ukurasa wa 11 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC, imeelezwa kuwa mtaji wa uwekezaji katika Mtambo wa IPTL ni Shilingi 50,000/= na kwamba huo ndio ungetumika kukokotoa Capacity Charges ili kulipa tozo ndogo kuliko ilivyo sasa.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Maelezo hayo siyo sahihi. Ukweli ni kwamba kutokana na maamuzi ya ICSID 1 ya tarehe 12 Julai, 2001, gharama za ujenzi wa Mtambo wa Tegeta ni Dola za Marekani 127.20 kama ilivyoelezwa katika Ukurasa wa 47 Aya ya 4 ya Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Katika Taarifa hiyo, pia imeelezwa kuwa ilikubalika kuwa uwiano wa deni na mtaji utakuwa 70:30. Hii ikiwa na maana kwamba, deni ni Dola za Marekani milioni 89.04 na mtaji ni Dola za Marekani milioni 38.16. Uamuzi huo haujabadilishwa na Mahakama yo yote au mtu ye yote.
Mheshimiwa Spika, Tunakubaliana kwamba fedha iliyopokelewa kutoka Mabenki ya Ushirika ya Malaysia kama mkopo ni Dola za Marekani milioni 85.86 ambazo kati ya Dola za Marekani milioni 105 zilizokuwa zimeidhinishwa. Swali la kujiuliza, je Mtambo huo ulikamilikaje kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 85.86, huku gharama halisi ya ujenzi wa Mtambo wa Tegeta ikawa Dola za Marekani milioni 127.20?
Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba kuna matumizi ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 38.16 ambazo pia zimetumika kwenye uwekezaji. Taarifa ya Kamati ya PAC haikuonesha fedha hiyo kuwa sehemu ya uwekezaji.
|
Mheshimiwa Spika, Tarehe 30 Juni, 2004, Kampuni ya Mawakili iliyokuwa ikiiwakilisha TANESCO katika kesi ya kwanza ya usuluhishi, Kampuni ya Mkono & Co Advocates, iliishauri TANESCO iendelee kupinga kiwango cha malipo ya Capacity Charge kilichokuwa kimeafikiwa tarehe 12 Julai, 2001 na pande hizi mbili katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) ya London. Hii ilikuwa ni miaka miwili tu baada ya usuluhishi uliochukua miaka minne kukamilika na Mtambo kuanza kuzalisha umeme tarehe 15 Januari, 2002.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo, baada ya ushauri huu, Mawakili hawa (Mkono & Co. Advocates) hawakuishauri TANESCO ifungue kesi katika Mahakama za Tanzania wala katika Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kimataifa (ICSID) ya London.
Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia tarehe 5 Septemba, 2013 wakati Mheshimiwa Jaji Utamwa anatoa hukumu yake juu ya mgogoro wa Wanahisa wa IPTL hapakuwepo na kesi yo yote kwenye Mahakama yo yote ya kupinga gharama za Capacity Charge kati ya TANESCO na IPTL, iwe katika Mahakama za ndani au za nje. Kwa kutokuwepo Msuluhishi (Broker) katika suala hili, madai yo yote ya TANESCO yanakuwa ni madai ya upande mmoja ambayo kisheria hayawezi kuchukuliwa kuwa ndiyo madai halisi. Kwa sababu hiyo haikuwepo formula rasmi ya kuutatua mgogoro huo zaidi ya majadiliano na maafikiano kati ya pande mbili (TANESCO na IPTL).
4. Uuzaji wa Hisa za VIP
Mheshimiwa Spika, Kutokana na VIP Engineering and Marketing Limited (VIP) kuona kuwa hainufaiki na ubia wake katika IPTL, ilikusudia kuuza Hisa zake kwa MECHMAR. Hata hivyo, MECHMAR haikuweza kununua Hisa hizo kwa sababu ilitaka thamani ya Hisa za VIP zitokane na ripoti ya ukaguzi ya mwaka (Audited Financial Report) na taratibu za kihasibu za kimataifa (International Accounting Rules), VIP haikukubaliana na utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na kutokubaliana, MECHMAR iliishauri VIP ifungue Shauri la madai hayo kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Uingereza (LCIA) kulingana na Mkataba wa Wanahisa wa IPTL. Hata hivyo, VIP haikufungua Shauri katika Mahakama ya usuluhishi kama ilivyoshauriwa na MECHMAR badala yake tarehe 25 Februari, 2002 VIP ikafungua Shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania (Miscellaneous Civil Application No. 49/2002) ikiomba Kampuni ya IPTL ifilisiwe ikiwa ni mwezi mmoja tangu kuanza uzalishaji.
5. Uamuzi kuhusu Ufilisi wa IPTL
Mheshimiwa Spika, Shauri lililofunguliwa na VIP tarehe 25 Februari, 2002 liliendelea kuwa Mahakamani hadi ilipofika tarehe 16 Desemba, 2008. Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya Jaji Oriyo, J ilitoa uamuzi wa kuiweka IPTL katika Ufilisi wa Muda (Provisional Liquidation) chini ya Kabidhi Wasii Mkuu (Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini – RITA). Mfilisi wa Muda alipewa majukumu maalum yafuatayo:
i. Kulinda mali zote za IPTL katika kipindi chote cha Ufilisi wa Muda; na
ii. Kufanya uchunguzi wa tuhuma zote zilizotolewa na VIP dhidi ya MECHMAR na kutoa ripoti za uchunguzi huo ili Mahakama iweze kutoa uamuzi.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 15 Julai, 2011, Mahakama Kuu ya Tanzania (Kaijage, J) ilitoa uamuzi kwamba, IPTL iwekwe kwenye Ufilisi Kamili (Full Liquidation) na RITA ilithibitishwa kuwa Mfilisi wa IPTL.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Standard Chartered BankHong Kong (SCBHK) iliyokuwa imenunua deni la IPTL kutoka kwa DANHARTA, ilipinga na kuiomba Mahakama ya Rufaa ifanye mapitio ya uamuzi wa Mahakama Kuu (Application for Revision – Civil Revision No. 1/2012) ikiainisha dosari katika uamuzi wa Mahakama Kuu ulioamuru kufilisiwa kwa IPTL. SCBHK ilibainisha dosari za maombi ya kutaka IPTL kufilisiwa kwa kuwa maombi ya SCBHK ya kutaka Mahakama iteue msimamizi (Administrator) wa kuisimamia IPTL (kwa niaba ya SCBHK) yalikuwa hayajasikilizwa.
Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilikubaliana na hoja za SCBHK na hivyo kuamuru shauri hilo lirejeshwe Mahakama Kuu ili IPTL irudi mikononi mwa Mfilisi wa Muda (Provisional Liquidator) ambaye alipewa majukumu yafuatayo:-
i. Kukusanya mali na madeni yote ya IPTL;
ii. Kupokea na kusajili madeni yote dhidi ya IPTL;
iii. Kusuluhisha migogoro kati ya wanahisa wa IPTL; na
iv. Kusimamia na kuendesha Mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL kwa niaba ya IPTL.
Mheshimiwa Spika, Baada ya kuteuliwa, Mfilisi wa Muda (Provisional Liquidator) alifanya juhudi ya kumaliza mgogoro huo wa IPTL nje ya Mahakama kwa kushirikisha wadau mbalimbali (Stakeholders) wa IPTL kupitia kikao chake cha tarehe 9 Novemba, 2011. (Kiambatisho Na.1). Juhudi hizo hazikufanikiwa na ikalazimu shauri liendelee Mahakamani.
6. Uhalali wa uhamishwaji wa Asilimia 70 za
Hisa za MECHMAR kwenda PAP
Mheshimiwa Spika, Suala la uhalali wa umiliki wa Hisa katika Kampuni hizi linahusu wanahisa wa Kampuni wenyewe. Serikali haiwajibiki kuingilia mahusiano ya kibiashara ya wanahisa katika Kampuni Binafsi. Hata hivyo, kulingana na Sheria za nchi ikiwa ni pamoja na Kifungu cha 172 cha Sheria ya Makampuni (Sura 212), mauziano ya Hisa yaliyofanyika nje ya nchi yatatambuliwa tu, endapo usajili wa Hisa hizo utafanyika hapa nchini. Kwa mujibu wa taarifa za BRELA za tarehe 31 Desemba, 2013, zinaonesha kuwa uhamishaji wa Hisa 7 za MECHMAR katika IPTL kwenda PAP ulisajiliwa hapa nchini. Kwa maana hiyo, PAP ni mmiliki wa Asilimia 70 za IPTL.
Katika ukurasa wa 44 Aya ya 1 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa PAP siyo mmiliki halali wa Hisa 7 za MECHMAR katika IPTL.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Katika maelezo ya Kamati ukurasa wa 30, Kamati imethibitisha kwamba nyaraka za mauziano kati ya MECHMAR na Piper Link zilipokelewa na Harbinder Singh Sethi ambaye pia ndiye mmiliki wa PAP. Kwa uthibitisho huo, Kamati inakubali kuwa Hisa za MECHMAR katika IPTL zinamilikiwa na PAP.
|
Katika Ukurasa wa 25 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa hakuna ushahidi wa PAP kumiliki Asilimia 70 ya Hisa zilizokuwa zikimilikiwa na MECHMAR katika IPTL.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa umiliki wa Hisa 7 za IPTL unatambuliwa hata na SCBHK ambayo ilisaini makubaliano tarehe 25 Novemba 2011 na PAP ya kulipwa deni la mkopo wa fedha za kununua deni la ujenzi wa Mtambo wa Tegeta. Kiambatisho Na 2.
|
7. Majadiliano ya mikopo ya IPTL na Wadai
Mheshimiwa Spika, Kutokana na Hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotolewa tarehe 5 Septemba 2013, Kampuni ya PAP ilijadiliana na wadai halali wa mikopo ya IPTL na kuingia Mkataba wa kuwalipa wadai wote wa IPTL. SCBHK inayodai kuidai IPTL mikopo katika ujenzi wa Mtambo wa Tegeta haikuwasilisha madai ya aina yo yote ili iweze kulipwa.
Mheshimiwa Spika, Ukweli ni kwamba, SCBHK iliyokuwa ikiidai IPTL fedha ilizotumia kununua deni lililotokana na kufilisiwa kwa MECHMAR kule Malaysia (siyo Tanzania) haijawahi kujadiliana na IPTL kuhusu malipo ya mkopo wake kama upo. Mvutano huu unaendelea ICSID kati ya TANESCO na SCBHK, ukiitaka TANESCO ilipe gharama za kununua umeme ikijumuisha deni la IPTL. Madai ya SCBHK dhidi ya TANESCO yanatokana na madai ya kuwepo kwa Deed of Assignment ya MECHMAR kuhusiana na Mkopo wa IPTL ambapo Mtambo wa IPTL uliwekwa kama dhamana ya Mkopo.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo Deed of Assignment hiyo haikuwahi kusajiliwa hapa nchini kama inavyotakiwa katika Kifungu Na. 172 cha Sheria za Makampuni Sura. 212 zinavyoelekeza. Kutokana na kutokusajili Assignment Deed hiyo, SCBHK ilikosa sifa za kufungua madai yake hapa nchini badala yake ilifungua madai haya ICSID nchini Uingereza. Kitendo hicho kinaonesha kudharau Mahakama zetu na PAC inataka tuziamini Mahakama za nje kuliko za kwetu.
8. Jitihada za Makampuni mbali mbali kununua Hisa za VIP
Mheshimiwa Spika, Kutokana na tofauti zilizokuwepo kati ya MECHMAR na VIP kuanzia mwanzo wa mradi, VIP iliamua kuuza Hisa zake zilizoko IPTL kwa makampuni mbalimbali kwa nyakati tofauti ikiwemo MECHMAR kama mwanahisa mwenzake, NSSF, Camel Oil, Great White Shark Opportunity Fund pamoja na SYMBION lakini haikuwezekana kutokana na kutoafikiana katika bei.
Mheshimiwa Spika, Baadaye VIP chini ya usuluhishi ya RITA, iliuza Hisa zake kwa PAP kwa thamani ya Dola za Marekani milioni sabini na tano (US$ 75,000,000/=). Ununuzi wa Hisa Asilimia 30 za VIP uliofanywa na PAP ndiyo uliyomaliza mgogoro wa Wanahisa uliyokuwa Mahakamani na kuufanya Mtambo wa IPTL kumilikiwa na PAP kwa kuwa ndiyo iliyomiliki Hisa zote Asilimia 100 za IPTL.
Taarifa ya PAC: Katika ukurasa wa 58 wa Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini ndiye aliyekuwa Dalali Mkuu aliyewakutanisha Bw Harbinder Sethi na Bw James Rugemalira
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Taarifa hii siyo sahihi kwa kuwa tangu tarehe 9 Novemba, 2011, RITA aliitisha mkutano na kuwakutanisha wadau wote wa IPTL. Wakati huo, Waziri wa Nishati na Madini aliyeko sasa alikuwa bado hajateuliwa kwenye wadhifa huo.
|
9. Kufungua ESCROW Akaunti
Mheshimiwa Spika, Tarehe 30 Juni 2004, TANESCO kwa ushauri wa Mkono & Co Advocates walitoa hoja kuwa gharama za kununua umeme zilikokotolewa kwa kutumia IRR ya Asilimia 23.10 na makadirio ya gharama za mtaji wa Asilimia 30 ambao ni Dola za Marekani milioni 38.16, wakati mtaji halisi (equity)wa IPTL ni chini ya Dola za Marekani 100. Hivyo, TANESCO walikuwa wakitoa notisi (Dispute Notice) kwa kila Ankara ya malipo kupinga gharama hiyo kulingana na Kifungu Na. 6.8 cha Mkataba wa PPA. Kifungu hicho kinaeleza kuwa ikiwa upande wote haukubaliani na usahihi wa malipo katika Ankara zilizowasilishwa kwa ajili ya malipo ya gharama za umeme wanatakiwa watoe notisi (Invoice Dispute Notice) kwa upande mwingine. Vile vile, Mawakili wa TANESCO (Mkono & Co Advocates) walishauri kwamba kutokana na pingamizi hilo, ifunguliwe Akaunti Maalum (Escrow Account) kwa ajili ya kuhifadhi fedha ambazo zilitokana na Ankara zilizokuwa zinapingwa.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na ushauri wa Mkono Co. & Advocates tarehe 5 Julai, 2006, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilisaini Mkataba wa kufungua Akaunti Maalum (Escrow Account)kwa ajili ya kuweka fedha zote za Ankara zilizopaswa kulipwa kwa IPTL.
10. Mmiliki wa Fedha za Akaunti ya Escrow:
Mheshimiwa Spika, Katika Taarifa ya Kamati ya PAC ukurasa wa 22 imeelezwa kuwa Akaunti ya Escrow ilipaswa kuwa na Shilingi bilioni 306.70 ambazo zingekuwa zimewekwa na TANESCO. Hata hivyo, katika mapendekezo ya Kamati ya PAC ukurasa wa 50, Kamati imeeleza kwamba imethibitisha bila chembe ya mashaka kwamba mchakato mzima wa kutoa fedha katika Akaunti ya Escrow umegubikwa na mchezo mchafu na kwamba Mfumo mzima wa Serikali ulipata ganzi ili kuwezesha zaidi ya Shilingi bilioni 306 kuporwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania na kutakatishwa kupitia benki mbili hapa nchini.
11. Tahadhari iliyochukuliwa na Serikali
wakati wa kutoa fedha kwenye akaunti ya
Escrow
Mheshimiwa Spika, Kwa kuelewa kwamba kunaweza kukatokea madai kwa IPTL, na kwa kuwa Serikali ilitoa dhamana kwa TANESCO ya kununua umeme wa IPTL, Serikali ilihakikisha inachukua KINGA(Indemnity) kutoka IPTL katika maeneo yote muhimu. Kwa mujibu wa KINGA hiyo, kama kutajitokeza madai yo yote yale, IPTL yenyewe itawajibika. Ikumbukwe kuwa kabla ya kusaini, KINGA hiyo ilipitiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuthibitisha kwamba inakidhi matakwa ya kulinda maslahi ya Taifa. KINGA hii ilitolewa tarehe 27 Oktoba, 2013. Inasema, nanukuu:
“IPTL do hereby agree to INDEMNIFY and keep INDEMNIFIED the Government and the Escrow Agent (jointly and severally) against all present and future claims, actions and legal proceedings that may arise in respect of and/or all losses, charges, costs, and expenses the Government and the Escrow Agent may suffer or incur consequent upon the release and payment of the funds in the Tegeta Escrow Account or part thereof to IPTL pursuant to the Agreement for Delivery of Funds”.
Katika Ukurasa wa 48 wa Taarifa ya PAC, imeelezwa kuwa Serikali haikuchukua tahadhari ya kutosha dhidi ya madai mengine yanayoweza kujitokeza kabla ya kutolewa kwa fedha kutoka akaunti ya Escrow.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, KINGA iliyochukuliwa inakidhi matakwa ya kisheria na imezingatia athari yo yote ambayo ingeweza kutokea baadaye kutokana na kutolewa kwa fedha katika Akaunti ya Escrow. Kwa hiyo siyo kweli kwamba Serikali haikuchukua tahadhari kama ilivyodaiwa na PAC.
|
12. Dhana ya Madai ya Shilingi Bilioni 321
Mheshimiwa Spika, Madai ya kwamba TANESCO inaidai IPTL Shilingi bilioni 321 msingi wake ni dhana kwamba mtaji wa IPTL ni Dola za Marekani 100, sawa na Shilingi za Tanzania 50,000/- kwa wakati huo. Dhana hii ilipuuza ukweli kwamba Dola za Marekani milion 38.16 ziliwekezwa kwenye mradi wa Tegeta. Aidha, Bodi ya TANESCO imekana kuyatambua madai hayo ya Shilingi bilioni 321. Kimsingi hata Vitabu vya Hesabu vya TANESCO ambavyo vimekuwa vikikaguliwa na CAG, havioneshi kuwepo kwa deni hilo.
Mheshimiwa Spika, Madai ya Shilingi bilioni 321 yaliyowasilishwa kwa Mfilisi na Mwanasheria wa TANESCO (Mkono & Co. Advocates) ulihitaji kuhakikiwa kabla ya kukubaliwa na Mfilisi kama madai halali. Hata hivyo, uhakiki huo haukufanyika kwa sababu ya Hukumu ya Mahakama ya Rufaa katika Civil Revision No. 1 ya Mwaka 2012, ambayo ilifuta maamuzi ya Mahakama Kuu ya kuiweka IPTL katika Ufilisi na kuirudisha kwenye Ufilisi wa Muda. Hivyo, madai hayo ya Shilingi bilioni 321 na kiapo chake ambacho hakitambuliwi na Bodi ya TANESCO hayakuwa tena na uhalali wo wote.
Kamati ya PAC: Katika ukurasa wa 47 Aya ya 2 Kamati imejiridhisha kuwa madai ya TANESCO ya Shilingi Billioni 321 yana uhalali japo usahihi wake utapatikana baada ya kutekelezwa kwa uamuzi wa ICSID 2 na TANESCO na IPTL kukubaliana kiwango sahihi cha Capacity Charge.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Madai ya kwamba TANESCO inaidai IPTL Shilingi bilioni 321 msingi wake ni dhana kwamba mtaji wa IPTL ni Dola za Marekani 100, sawa na Shilingi za Tanzania 50,000/- kwa wakati huo. Dhana hii ilipuuza ukweli kwamba Dola za Marekani milion 38.16 ziliwekezwa kwenye mradi wa Tegeta. Aidha, Bodi ya TANESCO imekana kuyatambua madai hayo ya Shilingi bilioni 321. Kimsingi hata Vitabu vya Hesabu vya TANESCO ambavyo vimekuwa vikikaguliwa na CAG, havioneshi kuwepo kwa deni hilo.
|
13. TANESCO na IPTL kufanya Reconcillation ya fedha iliyokuwa kwenye Akaunti ya Escrow
Mheshimiwa Spika, TANESCO kwa kushirikiana na IPTL ilifanya uhakiki (reconciliation) tarehe 9 Oktoba, 2013 ili kujua madai halali ya IPTL kabla ya kufanya malipo. Takwimu za Mfilisi wa Muda wa IPTL (RITA) wakati akikabidhi mali na madeni ya IPTL, ilionesha kwamba deni lote alilokuwa akidaiwa TANESCO na IPTL kama Capacity Charges ni Shilingi bilioni 370.70, sawa na Dola za Marekani milioni 224.30. Katika majadiliano kati ya TANESCO na IPTL, gharama zilizokubaliwa kama Capacity Chargeszilizokuwa zinadaiwa ni Shilingi bilioni 275.20. Fedha hizi ni pungufu kwa Shilingi bilioni 95.50 ya madai ya IPTL. Hadi kufikia tarehe 25 Novemba 2013, fedha iliyokuwa katika Akaunti ya Escrow ilikuwa jumla ya Dola za Marekani milioni 22.20, sawa na Shilingi bilioni 36.72 na Shilingi bilioni 161.39.
Mheshimiwa Spika, Ukaguzi maalum umeonesha pia kuwa fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow wakati wa kuifunga ni Shilingi bilioni 182.77 na kuwa na upungufu wa Shilingi bilioni 123.90 wa madai ya IPTL.
14. Iwapo Serikali ilistahili kutoa fedha katika Akaunti ya Escrow wakati Shauri la ICSID, London inaendelea
Mheshimiwa Spika, Kesi iliyopo ICSID, London ilihusu madai ya Benki ya Standard Chatered ya Hong Kong yaliyotokana na kununua deni lililotokana na uwekezaji katika Mtambo wa IPTL wa Tegeta. Katika Mkopo huo, Mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na Mtambo wa kuzalisha umeme wa Tegeta viliwekwa kama dhamana.
Mheshimiwa Spika, TANESCO haikuhusishwa kwenye majadiliano ya dhamana hiyo. IPTL ilishindwa kumaliza marejesho ya Mkopo huo na hivyo Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong kuanza kuidai TANESCO madeni yaliyotokana na Mkopo huo. Hata hivyo, fedha katika Akaunti ya Escrow ilitokana na Ankara za Capacity Charges zilizokuwa zikibishaniwa kati ya TANESCO na IPTL kuhusu viwango vilivyotumika kukokotoa malipo hayo na siyo mikopo ya IPTL.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo, Standard Chartered Bank Hong Kong siyo mhusika (not a party) katika Mkataba wa tarehe 26 Mei, 1995 wa PPA kati ya TANESCO na IPTL. Kwa mujibu wa Sheria za Tanzania, madai yo yote yaliyotokea nje ya nchi yakihusu uwekezaji ulioko nchini ni lazima yasajiliwe hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kwa mantiki hiyo, Shauri lililoko ICSID, London halihusiani na fedha za Akaunti ya Escrow bali mikopo ya IPTL. Hata hivyo, wadai wa IPTL waliamriwa na Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 5 Septemba, 2013 kuwasilisha madai yao kwa PAP. Benki ya Standard Chatered ya Hong Kong haijafanya hivyo.
15. Ulipwaji wa Madai na Madeni
Mheshimiwa Spika, Kuhusu madai na madeni dhidi ya IPTL ikiwemo VAT, Serikali na BOT ziliitaka IPTL iweke KINGA (Indemnity) ili kuihakikishia Serikali kuwa endapo kutakuwa na madai au madeni ya aina yo yote, IPTL itawajibika kuyalipa. Tarehe 27 Oktoba, 2013, IPTL ilitoa KINGA hiyo, nanukuu:
“IPTL do hereby agree to INDEMNIFY and keep INDEMNIFIED the Government and the Escrow Agent (jointly and severally) against all present and future claims, actions and legal proceedings that may arise in respect of and/or all losses, charges, costs, and expenses the Government and the Escrow Agent may suffer or incur consequent upon the release and payment of the funds in the Tegeta Escrow Account or part thereof to IPTL pursuant to the Agreement for Delivery of Funds”.
16. Gharama za Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams ya Marekani) Katika Kuendesha Kesi za IPTL
Mheshimiwa Spika, Hadi Hukumu ya Mheshimiwa Jaji Utamwa inatolewa tarehe 5 Septemba mwaka 2013, TANESCO na Serikali zilikuwa zimewalipa Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) jumla ya Shilingi za Tanzania bilioni 62.90 na bado Mawakili hawa (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) wanaidai TANESCO Dola za Marekani milioni 4.50. Katika ushauri wao walikuwa wamependekeza kwa Serikali wapewe kazi nyingine ya kwenda kutetea Guarantee ya Serikali pamoja na kupinga Hukumu ya tarehe 12 Februari, 2014 iliyotolewa katika uamuzi wa ICSID-2. Ushauri wao upo katika Memorandum ya tarehe 9 Oktoba, 2013 waliyowasilisha TANESCO.
Mheshimiwa Spika, Wakati ambapo hatukujua ni kiasi gani Serikali na TANESCO ingeweza kupata kwa kuendelea kupinga Capacity Charges za IPTL, tunajua fika ni hasara gani tumepata kupitia malipo ya Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) yaani ya Shilingi bilioni 62.9 na bado wanadai Dola za Marekani milioni 4.5.
Mheshimiwa Spika, kumalizika kwa mgogoro huu wa IPTL si tu kwamba kumetuondoa kwenye hatari ya kuendelea kukamuliwa na Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) hawa bali pia katika mazungumzo yaliyofanywa kati ya TANESCO na IPTL tumeweza kuokoa takribani Shilingi bilioni 95 katika madai ya awali ya IPTL.
17. Ushauri wa Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) wa TANESCO wa Tarehe 4 Oktoba, 2012
Mheshimiwa Spika, Mawakili wa TANESCO na Serikali yaani Kampuni za Mkono & Co Advocates na Hunton & Williams waliandika ushauri wa pamoja wa tarehe 4 Oktoba 2012 ambapo walifafanua kwa kina juu ya Shauri lililokuwa likiendelea katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) ya London. Katika Ushauri wao walionyesha wazi kwamba TANESCO ilikuwa na nafasi finyu mno ya kushinda katika Kesi iliyokuwa ikiendelea kati ya TANESCO na SCBHK.
Mheshimiwa Spika, Katika ushauri wao walieleza mambo muhimu ambayo ni vema Bunge lako Tukufu likAyaelewa hasa kwa ajili ya watu wanaodhani kwamba ilikuwa ni makosa kwa TANESCO kukaa na IPTL baada ya Hukumu ya Mahakama Kuu ya tarehe 5 Septemba, 2013. Baadhi ya maeneo walioshauri TANESCO ikae na IPTL kujadiliana kwa kile kilichoelezwa na Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) kuwa uwezekano wa kushinda kesi ni mdogo ni pamoja na:-
18. Ushauri wa Mawakili Unaokinzana
Mheshimiwa Spika, Tarehe 4 Oktoba, 2012, Mawakili wetu (Mkono & Co. Advocates na Hunton & Williams) walitoa ushauri kwamba

No comments:
Post a Comment