WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewasili jijini Doha, Qatar jana usiku (Jumamosi,
Desemba 20, 2014) kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Serikali ya nchi
hiyo inayotarajiwa kuanza leo.
Lengo
la ziara ya Waziri Mkuu ni kukuza mahusiano baina ya nchi hizi mbili,
kuangalia fursa za kiuchumi na miradi mikubwa inayoweza kuzinufaisha
nchi hizo na nje ya mipaka yake kwenye Ghuba ya Arabuni (Arabian Gulf)
na bara la Afrika.
Vile
vile Waziri Mkuu anatarajiwa kutangaza fursa za uwekezaji nchini
Tanzania, fursa za biashara, za utalii na kutafuta mitaji kwa ajili ya
sekta za uchimbaji gesi na mafuta, usindikaji mazao, uvuvi na mifugo,
ajira na uendelezaji miundombinu.
Kwa
mujibu wa ratiba iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Waziri Mkuu atakuwa na mazungumzo ya kiserikali na Waziri
Mkuu wa nchi hiyo, Sheikh Abdulla Nasser Al Thani. Vilevile atakutana na
Mawaziri wa Kazi na Ustawi wa Jamii; Uchukuzi; Miundombinu na Uwekezaji
wa nchi hii. Naibu Mawaziri atakaokutana nao ni wa Uchumi na wa
Nishati.
Vilevile
Waziri Mkuu amepangiwa kukutana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wafanyabiashara wa Qatar (Qatar Business Community), wajumbe wa Chama
cha Wafanyabiashara cha Qatar (Chamber of Commerce of the State of
Qatar) na pia atakutana na Watanzania waishio Qatar. Atatembelea pia
Mamlaka ya Bandari ya Qatar na makao makuu ya kampuni ya uchimbaji gesi
ya Qatar.
Waziri
Mkuu amefuatana na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus
Kimani; Waziri wa Kilimo na Maliasili wa Zanzibar, Dk. Sira Ubwa
Mamboya; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw.
Mahadhi Maalim; Naibu Waziri wa Nishati, Bw. Charles Kitwanga; Naibu
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Godfrey Zambi.
Wengine
ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,
Bi. Halima Dendego, wabunge wawili Bi. Amina Makilagi na Bw. Aeshy
Hilali na wakuu wa taasisi za TPSF na TPDC.

No comments:
Post a Comment