Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe.
Bernard Membe, amesema leo kuwa hakuna Mtanzania kati ya watu wanane
waliouwawa katika mashambulizi dhidi ya wageni huko Durban na
Johannesburg nchini Afrika ya Kusini.
Mhe. Membe amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa
taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba Watanzania
watatu wameuwawa katika mashambulizii hayo siyo za kweli.
"Nimehakikishiwa na Waziri wa Usalama wa Afrika kusini, David
Mahlobo, asubuhi hii kuwa hakuna Mtanzania kati ya watu wanane
waliouwawa, ambao ni raia wa Ethiopia, Zimbabwe, Malawi na Swaziland,"
ametaarifu Mhe. Waziri.
Amesema serikali ina taarifa kuwa kuna Watanzania watatu waliofariki
dunia nchini Afrika Kusini, lakini hawakuuwawa katika mashambulizi ya
wenyeji dhidi ya wageni.
"Watanzania hao ni Rashidi Jumanne, ambaye imetaarifiwa alipigwa risasi
katika tukio la ujambazi, kilometa 90 nje ya mji wa Durban; mfungwa
Athumani China Mapepe, aliyeripotiwa kuchomwa kisu gerezani wakati wa
vurugu za wafungwa, na Ali Heshima Mohamed, ambaye alifariki hospitalini
kutokana na ugonjwa wa TB," alieleza Mhe. Membe.
Mwili wa marehemu Mohamed ulirejeshwa nchini jana kwa
mazishi. Mhe. Waziri alitaarifu kuwa kuna Watanzania 23 katika kambi
iliyotayarishwa na serikali ya Afrika Kusini huko Durban kuhudumia
wageni wanaokimbia mashambulizi hayo ya wenyeji, na kuwa utaratibu
unafanywa kuwarejesha nyumbani raia 21 walioomba. "Wawili wamesema
hawako tayari kurudi."
Mhe. Membe amesema taarifa ya serikali ya Afrika Kusini inaonyesha kuwa
hali ya utulivu imerejea Durban na Johannesburg katika saa 48 zilizopita
kutokana na juhudi za Rais Jacob Zuma na kamati maalum ya mawaziri
aliyoiteua kushughulikia mashambulizi hayo.
Mapema jana, Mhe. Membe alimwita Balozi wa Afrika Kusini nchini
Tanzania, Mhe. Thamsanqa Dennis Mseleku, na kuelezea kukerwa kwa
serikali na mauaji ya wageni na akataka hatua madhubuti zichukuliwe
kuhakikisha usalama wa Watanzania nchini Afrika Kusini.
Alisema Tanzania inaunga mkono taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Robert Mugabe wa
Zimbabwe, ambayo imelaani vikali mashambulizi ya Waafrika kutoka nje ya
Afrika Kusini. Hata hivyo, Rais Mugabe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Umoja wa Afrika (AU), amesifia hatua zinazochukuliwa na serikali ya
Afrika Kusini kukomesha mashambulizi hayo na kurejesha utulivu.
Mhe. Membe aliwataka Watanzania waishio Afrika Kusini na kwingineko nje
ya nchi, kujitambulisha kwenye balozi zetu ili iwe rahisi kufuatilia
usalama wao na kuwasaidia pale yatokeapo majanga.
"Hatuna takwimu sahihi za idadi ya Watanzania waishio Afrika kusini kwa
sababu wengi wao wamekwenda huko kwa njia za panya," alisema.
Inakadiriwa kuna Watanzania 10,000 waishio Johannesburg na Durban.
Akijibu swali la mwandishi wa habari, Mhe. Membe alisema Tanzania
inapaswa kutumia utajiri mkubwa wa gesi asilia ilionao ili kuendeleza
viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vitakavyotengeneza ajira za kuvutia
kwa vijana ili wasikimbilie nchi za nje na kuhatarisha maisha yao.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
20 Aprili 2015 |
No comments:
Post a Comment