Monday, 4 May 2015

MAALIM SEIF SHARIFF AKABIDHIWA PESA ZA KUGOMBEA URAIS-ZANZIBAR

1
Mwenyekiti wa CUF zoni ya Mjini Unguja Massoud Khamis, akimkabidhi fedha taslim Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, ili aweze kuchukua fomu ya kugombea urais wa Zanzibar wakati utakapofika.
2
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akionyesha fedha alizokabidhiwa kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea urais.
3
Mwenyekiti wa CUF zoni ya Mjini Unguja Massoud Khamis, akimkabidhi Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, cheti cha heshima kutokana na uongozi wake..
45
  Baadhi ya viongozi na wanachama wa CUF waliojitokeza katika hafla ya kumkabidhi fedha Maalim Seif iliyofanyika nyumbani kwake Mbweni.
…………………………………………………………
                                           Na Maelezo-ZANZIBAR                                        

Uongozi wa Zoni ya Mjini wa Chama cha Wananchi CUF umemkabidhi Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Shariff Hamad Shl.Million mbili na Laki tano kwa ajili ya kuchukua Fomu ya kugombea Nafasi ya Urais Zanzibar wakati utakapofika.
Hafla ya kukabudhi Fedha hizo ilifanyia Jioni ya Jana Nyumbani kwa Maalim Seif Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na kuhudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Chama hicho.
Akikabidhi Fedha hizo Mwenyekiti wa Zoni ya Majini Masoud Khamis alisema wameamua kumlipia Kiongozi huyo baada ya kutangaza nia yake ya kugombea katika nafasi hiyo.
Aidha alisema kuwa wapo baadhi ya Watu wanadai Maalim Seif hatakiwi kugombea Nafasi hiyo kutokana na kujilipia Fomu kwa Pesa zake hivyo wameona ipo haja ya kumlipia ili kuonesha Mapenzi ya dhati kwake.
“Wanasema wewe Maalim hutakiwi unajitakisha ndio maana kila ufikapo muda wa uchaguzi Unajilipia Fomu mwenyewe kwa hiyo tunawajibu kuwa wewe ni chaguo letu na ni Mtu wa Watu” Alisema Mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad, amesisiza nia yake ya kugombea tena nafasi ya Urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao.
Maalim Seif ameishukuru kamati hiyo kwa uamuzi wa busara waliochukua, hali inayoonyesha kuwa wananchi wa Zanzibar wanaendelea kuwa na imani naye kutokana na mwelekeo wake wa kutaka kuleta mabadiliko ya kweli kwa Zanzibar.
Amesema iwapo wananchi watakipa ridhaa Chama hicho kuongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu,  kitatandika misingi imara ya utawala bora, uchumi na kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.
Ameyataja mambo mengine ya msingi kuwa ni pamoja na kurejesha heshima ya Zanzibar katika jamii ya Kimataifa, kuimarisha huduma za kijamii ziliwemo afya na elimu, pamoja kuandaa mazingira ya kuongeza ajira kwa vijana.
Amesema tofauti na chaguzi zilizopita, Chama hicho kimejiandaa vizuri kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, na kuwaomba wananchi waendelee kukiunga mkono ili kiweze kupata ushindi mkubwa na kuweza kuongoza serikali.
Mapema akisoma risala ya kamati maalum ya (CUF) zoni ya mjini, mjumbe wa kamati hiyo Bw. Salim Abdallah Salim amesema wameamua kumdhamini Maalim Seif kutokana na utendaji wake ndani ya chama hicho pamoja na matumaini aliyonayo kwa Wanzibari.
Aidha kamati hiyo imetoa tamko rasmi la kumuunga mkono Maalim Seif kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar wakati utakapofika, na kutoa wito kwa vijana kutafuta vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi (ZAN ID) na kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, ili waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.

No comments:

Post a Comment