Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (pichani) , amenusurika kifo
baada ya ndege aliyokuwa akisafiria kutoka Iringa kwenda Zanzibar kutaka
kugongana uso kwa uso na ndege nyingine dakika moja kabla ya kutua.
Waziri Membe akiwa na ujumbe
wake wa watu wanane, walikuwa wakisafiria ndege ya kukodi kampuni ya 5H
NEG Precition Aviation ikirushwa na rubani Mathew Mhahiki, ambaye
ameonyesha kushangazwa na tukio hilo alilodai “ni kwa rehema za Mungu
tumepona ajali hii.”
Akizungumza na mwandishi wetu
aliyeko katika ziara yake, rubani Mhahiki alisema: “Lazima kuna tatizo
katika control center hata hivyo tayari nimeongea nao na wameniomba
samahani na kudai walipitiwa, maana kwa hali ilivyokuwa ni kwamba
tungegongana wakati wa kutua maana nimeshangaa tu kuona ndege hii hapa
ndiyo maana nikaamua kumkwepa mwenzangu nikapanda juu.”
Waziri Membe alisema: “Nina
uzoefu mkubwa wa kusafiri na ndege mahali pengi duniani, hali hii
ilikuwa ni ajali na labda sasa tungekuwa dead bodies, lakini ninajua
Mungu yuko upande wetu katika safari hii ya uhakika, lakini pia
izingatiwe nimekuja kufanya kazi ya Mungu.”
“Katika safari hii tutashuhudia
mambo mengi sana, lakini kwa kuwa kila ninapotaka kuondoka nyumbani ama
hotelini mara nyingi nimekuwa nikimtanguliza Mungu maana bila Mungu hii
ilikuwa ni mwisho wa maisha yetu tuliokuwa kwenye ndege hii.”
Waziri Membe alikuwa amealikwa
mjini hapa na Umoja wa Akimama wa Kikristu (Umaki) wa Kanisa la
Anglikana Dayosisi ya Zanzibar waliokuwa wakifanya mkutano wao mkuu
unaofanyika kila baada ya miaka mitano akitokea Iringa ambako alikwenda
kutafuta udhamini wa chama ili kumwezesha kugombea urais kupitia Chama
Cha Mapinduzi, CCM.
Akiwa uwanjani hapo, Waziri
Membe alikutana na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba aliyekuja hapa
Zanzibar kutafuta wadhamini ambapo makada hao walipata nafasi ya
kuzungumza.
Akiwa katika mkutano huo, Waziri
Membe alisema: “Miongoni mwa mambo yanayonikera ndani nafsi yangu ni
kuona mwanamke bado anaachwa nyuma, hili halipendezi, ni lazima
tuhakikishe wanawake wanapata elimu ya ufundi stadi maana mwanamke
akiwezeshwa hasa katika eneo hili la elimu wanaweza hata kushinda
wanaume wengi.”
“Ni lazima kina mama wawezeshwe
kujiajiri ili msiwategemee kina baba kwa kila jambo lakini pia ili
kufikia malengo hayo ni lazima tuwape elimu kina mama.”
No comments:
Post a Comment