Monday 20 July 2015

JAMAL RWAMBOW AGOMBEA UBUNGE JIMBO LA RUFIJI

download (1)
Dar es Salaam. Mjumbe wa Baraza la Michezo la Tanzania Bara (BMT), Jamal Mandenda Rwambow amerejesha fomu kuwania Ubunge wa Jimbo la Rufiji klupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza jijini jana, Rwambow ambaye ni mdau mkubwa wa michezo alisema kuwa sababu kubwa ya kuomba kuwatumikia wakazi wa jimbo la Rufiji ni kuleta maendeleo ya haraka katika kila sekta.
Alisema kuwa mbali ya sekta ya michezo, pia amepania kuwakwamua wakaji wa jimbo hilo katika hali ya umaskini waliyokuwa nayo hasa kwa kutumia utajiri wa rasilimali za jimbo hilo ikiwemo bonde la kilimo la mto Rufiji.
Alifafanua kuwa pamoja na kuweka nia ya kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya CCM, pia ameweka vipaumbele kadhaa ambavyo ndivuo vitawafanya wakazi wa jimbo hilo kupata maendeleo ya kina na si vinginevyo.
“Kwenye michezo nitasaidia timu na kuinua vipaji na kuviendeleza na kufikia hatua ya juu kabisa, jimbo la Rufiji lina wachezaji wengi wa mpira wa miguu, mpira wa kikapu, netiboli na michezo mingine, hata mabondia wapo katika jimbo hilo, hakuna mtu aliyeweza kuwatoa hapo walipo na kufikia kiwango cha kitaifa na kimataifa, kazi hiyo sasa itakuwa ya kwangu mimi,” alisema Rwambow.
Alisema kuwa aliwajengea uzio wa uwanja wa mpira wa miguu, hatua ambayo iliwawezesha wachezaji kuanza kufaidi matunda ya uchezaji wao baada ya kuanza kupata fedha kidogo kutokana na jasho lao.
Kuhusiana na sekta nyingine, Rwambow alisema kuwa nyenzo kuu ni kutafuta mitaji, kuweka mipango na kuitekeleza, kufanya kazi kama timu moja, kuyafanya mambo ya maendeleo kwa haraka zaidi na kutambua watendaji bora na kuwakemea wazembe.
“Nitahakikisha tunafanyakazi pamoja kwa vitendo na siyo kusema tu, hii itakuwa katika sekta zote ambazo ni muhimu kwa binadamu,” alisema.

No comments:

Post a Comment