Baada ya zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea ubunge kukamilika Majimbo yote yanatakiwa kuanza zoezi la kura ya maoni tarehe 20-25 Julai mwaka huu kwa kuzingatia Mwongozo wa Taratibu za Kura ya Maoni ambao umeshatumwa nchi nzima.
“Kwa majimbo ya yaliyogawanywa kila jimbo litafanya mchakato wake wa kura ya maoni kwa kusimamiwa na mamlaka zilizotajwa katika mwongozo husika. Hii maana yake ni kwamba zoezi la kura ya maoni litafanyika kwa siku 6 mfululizo. Kila kanda inapaswa kuweka ratiba yake ya ndani katika muda huo na kuhakikisha kuwa majimbo yote, ya zamani na mapya, katika kanda husika yakamilishe kura za maoni ndani ya tarehe hizo.
“Kamati Kuu iliazimia pia kuwa kura za maoni nafasi ya udiwani zitaanza kufanyika kuanzia tarehe 30 Julai hadi 5 Agosti, 2015. Hii maana yake ni kuwa zoezi la kura za maoni kwa nafasi ya udiwani litaanza baada ya kumalizika kwa zoezi la kura za maoni nafasi ya ubunge,” ameagiza Katibu Mkuu Dk. Slaa kupitia waraka huo.
Aidha Katibu Mkuu amewaagiza Waratibu wa Kanda za CHADEMA kusimamia utaratibu wa kuwatangazia wananchi katika majimbo yote kwa njia anuai ikiwemo vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, matangazo kwenye mbao na nafasi mbalimbali za hadhara ili Watanzania wote wapate fursa ya taarifa hiyo muhimu.
No comments:
Post a Comment