Tuesday, 14 July 2015

MBIO ZA KUWANIA NAFASI YA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ZAANZA KUTIMUA VUMBI DAR

magu
Dkt. John Pombe Magufuli akiwasili  katika viwanja vya Zakhem Mbagala ambako kumefanyika mkutano wa kumtambulisha kwa wananchi  leo jijini Dar es salaam.(Picha na Eleuteri Mangi –MAELEZO)
…………………………………………………………..
Na Eleuteri Mangi
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemtambulisha Mgombea wake wa Urais wa Jamhuri ya Muungano Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM 
  Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Mgombea Mwenza Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi kupitia wana mkoa wa Dar es salaam kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika leo jijini Dar es salaam.
Mkutano huo wa hadhara wa kumtambulisha Mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM unalenga maandalizi ya chama hicho kuelekea mbio za kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ili kuwania kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano nchini.
Akiongea na wananchi kupitia mkutano huo wa hadhara, Dkt. Magufuli amesema kuwa amefurahishwa kwa mapokezi mazuri ya wana Dar es salaam waliyomuonesha na ameahidi hatawaangusha akipewa ridhaa ya kuiongoza nchi mara baada ya uchaguzi mkuu wa Octoba 25 mwaka huu.
“Leo ni siku ya kutambulishwa tu, ni vema kuheshimu misingi imara iliyoasisiwa na viongozi wetu Mwl. Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume na kuendelezwa na viongozi waliopita na waliopo madarakani sasa kwa kudumisha amani na umoja wetu” alisisitiza Dkt. Magufuli.
Aidha, Dkt. Magufuli amesema kuwa maendeleo ya nchi hayana chama ambapo kila Mtanzania anahitaji maendeleo ya kweli yatakayolettwa kupitia sekta mbalimbali ikiwemo afya, viwanda, barabara, reli maji, elimu na sekta nyingine nchini.
Akifafanua kauli yake, Dkt. Magufuli amesema kuwa Watanzania wanahitaji maendeleo wamechoka kulalamika ambapo katika kusimamia adhma hiyo atasimamia vema ilani ya uchaguzi ya chama chake na kuhimiza kuwa anachukia watendaji wa Serikali wasiotimiza wajibu wao kitu ambacho atakisimamia ili kuboresha utendaji kazi kwa manufaa ya Watanzania wote.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana wakati akimkaribisha na kumtambulisha Mgombea huyo wa Urais kwa wananchi, amesema kuwa chama chake kimempata Mgombea ambaye ni zaidi ya jembe ambapo amemfananisha na tingatinga akiwa na adhma ya kusimamia na kuboresha maendeleo ya wananchi ili wanufaike na matunda ya nchi yao.
Uteuzi wa  Mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM na Mgombea mwenza wake ulifanywa na mkutano mkuu wa chama hicho mapema wiki hii mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kinyang’anyiro hicho awali kilikuwa na jumla ya watangaza nia 42 ambapo kati ya hao 38 ndiyo waliogia katika kinyang’anyiro hicho ambacho Dkt. Magufuli aliibuka kidedea.

No comments:

Post a Comment