Source http://mtanzania.co.tz/
NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe, ametangaza rasmi kutetea nafasi yake baada ya kuombwa kufanya
hivyo na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Pamoja na hilo, pia amewakaribisha wanachama wa Chadema wanaohisi wana uwezo wa kushinda nafasi hiyo kujipima kwake.
Alitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, baada ya kuchukuliwa fomu na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee
wa Mkoa wa Kigoma, Yasin Mzigo, kwa niaba ya viongozi wengine wa
mabaraza ya wazee alioambatana nao kutoka mikoa mbalimbali.
Baada ya Mbowe kupokea fomu hiyo ya kukubali kuingia kwenye
kinyang’anyiro cha kutetea kiti chake, aliwashukuru wazee hao na kueleza
sababu ya kukubali ombi lao la kumtaka awanie tena nafasi hiyo ya juu
ndani ya Chadema.
“Kuna mambo mawili yananipa wakati mgumu kukubali ombi hilo, kwanza
Chadema ni chama kilichosheheni watu wenye taaluma, uzoefu na weledi
mbalimbali, kwanini iwe mimi. La pili ni namna makundi mbalimbali
yalivyojitokeza kutaka niwanie uenyekiti hali inayoweza kutoa nafasi kwa
wapenda majungu kufikiria kwamba jambo hilo nimelipanga mimi,” alisema.
Alisema awali hakukusudia kugombea nafasi hiyo na ndiyo maana aliwahi
kutoa kauli ya kukataa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho mbele ya
kikao cha Kamati Kuu, ambapo aliwataka wanachama kumchagua mtu mwingine
akiongoze chama.
“Niliwaeleza kwamba nahitaji nimpate Mnyamwezi mwingine ili
nimkabidhi jiwe hili, lakini Kamati Kuu ilikataa na ikatoka na tamko la
kukataa kuachia uenyekiti, ingawa niliwaambia kwamba naacha nafasi hii
si kwa sababu naichukia Chadema na sio kwa sababu namwogopa mtu yeyote,
lakini ni kwa sababu nimekitumikia chama hiki kwa umri wangu wote na kwa
uadilifu.
“Na mimi ni binadamu, nina familia na maisha mengine, hivyo nahitaji
niendelee na maisha mengine, lakini kauli za viongozi wengine na makundi
mbalimbali zimekuwa za kunitaka kukubali wito wa kuchukua tena fomu, ni
kweli hadi sasa sijachukua fomu na kesho natarajia niondoke asubuhi
kwenda Uingereza na ninawashukuru wote walioona naweza kuongoza tena
chama hiki,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo alimweleza mwakilishi huyo wa wazee ambaye ndiye
aliyemchukulia fomu kwa niaba ya wanachama wengine wa Mkoa wa Kigoma
kuwa akiwa mpiganaji, amejikuta akipata wakati mgumu kutokana na
misimamo yake ya kupigania haki ya kutetea demokrasia, lakini katu
hatorudi nyuma kwa masilahi ya taifa.
Alisema kuwa katika maisha yake ndani ya Chadema, hajawahi kuomba
kuwania nafasi ya uenyekiti na badala yake amekuwa akiombwa kuwania
nafasi hiyo na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Akitolea mfano mwaka 2004, Mbowe alisema nafasi hiyo aliombwa kuwania
na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema marehemu, Bob Makani, ambaye alikuwa
anamaliza muda wake wa uongozi ndani ya chama hicho.
Pamoja na kutakiwa kufanya hivyo, alisema alikataa kutokana na
kubanwa na shughuli zake hali iliyofanya Bob Makani kuunda jopo la wazee
ambao walimchukulia fomu na kumtaka kujaza, akakubali kugombea.
Alisema mwaka 2005 wakamuomba tena kugombea baada ya mgombea
aliyekuwa amepitishwa kuwania nafasi hiyo na chama, Profesa Mwesiga
Baregu kujitoa dakika za mwisho.
Mbowe alisema kuwa hata mwaka 2009 aliombwa tena kuwania uenyekiti
akagoma, lakini wazee wa Dar es Salaam walimuomba tena, ikiwamo na
kumjazia fomu, lakini kwa mwaka huu imekuwa tofauti kwani fomu
amechukuliwa na wazee kutoka Kigoma.
Alitoa wito kwa wale wanaofikiria kwamba alitengeneza jambo hilo kwa
kusema: “Hata ninyi kama kuna mwandishi wa habari ana nia ya kuvuta fomu
avute tu, aone ngoma itakavyokuwa na anayetaka kujipima aje apime,
nawahakikishia hii ngoma nitaicheza tena na anayefikiria ana ubavu wa
kucheza ngoma hii ajitokeze,” alisema.
Mbowe alisema kuwa kuna changamoto nyingi za kuendesha chama cha siasa na wala hakuna raha kama inavyokuwa inafikiriwa na wengi.
“Ndugu zangu kazi ya kuongoza na kujenga chama cha siasa si mchezo,
ni kazi inayohitaji ‘commitment’ na si kazi ya ulaji kama wengi
wanavyofikiri kwamba Mbowe anatafuna ruzuku… ipi? Kazi hiyo ni ya hatari
kwani inakulazimisha wakati wote kutoonana na watoto wako, na unaweza
kuondoa maisha yako wakati wowote kama usipoifanya kwa uaminifu na
ujasiri, kwani hakuna jeshi wala silaha itakayosaidia,” alisema.
Aliongeza kuwa iwapo kazi hiyo itafanyika kwa uhakika, hata uadilifu na ulinzi wa Mungu utaupata kwa uhakika.
“Nimefanya kazi yangu kwa kujiamini sana, sina hofu ya usalama wa
jeshi, polisi au raia ninamuheshimu mdogo hadi mkubwa, mwenye mamlaka na
asiyekuwa nayo, lakini kamwe simwogopi yeyote, nadhani naweza kusema
hiyo ndiyo imekuwa silaha iliyoniwezesha kukifikisha Chadema hapa
kilipofika,” alisema.
Mbowe aliongeza kuwa kazi ya kukiimarisha chama kwa miaka 20
ameifanya kwa kushirikiana na wapambanaji wengine, lakini wapo
aliowaacha njiani kwa kutokujua na wengine kwa kutumika huku wengine
wakipotea kwa kuishiwa nguvu.
“Wapo waliofanikiwa kujenga umashuhuri kwa kupitia chama hiki na
kupata senti mbili tatu, basi wanaona malengo yao yametimia, lakini
yangu na wengine ni kuhakikisha taifa hili linapata viongozi waadilifu
wenye kuwajali wananchi wote wakiwamo maskini,” alisema.
Akizungumzia viongozi wanaojiuzulu nyadhifa zao katika chama hicho,
Mbowe alisema kuondoka kwao kumechangiwa na kukimbia mbinu mpya
zilizobadilishwa na chama hicho za viongozi wa juu kuchaguliwa na
wanachama.
Alisema sababu hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kwa sasa chama hicho
kuwa tofauti na vingine, kutokana na kuanza kuwajengea hamasa wananchi.
Mbowe alikimwagia sifa Chadema kwa kusema kuwa amekijenga kwa weledi
na kukifanya kuwa tofauti na kilivyokuwa hapo nyuma ambako viongozi wa
mikoani walikuwa wakipeana nafasi.
“Nikifanikiwa kuwa mwenyekiti wa chama hiki, naamini nitakuwa
nimekwenda kukiongoza chama ambacho kina mtandao ambao haujawahi kutokea
katika chama chochote cha siasa nchini,” alisema.
Kuhusu kauli za kubomoka kwa Chadema, Mbowe alipinga na kusema kwa
sasa chama hicho kipo imara na ukweli huo utathibitishwa kwenye
uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu ujao.
“Watauelewa muziki wa Chadema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na
kuona namna tulivyojenga mtandao wa chama na oganaizesheni, sisi
hatujengi majengo bali tunajenga fikra za watu nchi nzima, kwani kazi ya
kujenga ofisi si kazi ya chama hiki, kwani kipaumbele ni kujenga fikra
za wananchi kudai haki zao na wale wanaosema dhaifu hawaielewi Chadema,”
alisema.
Mbowe aliongeza kuwa Chadema mpya itaonekana Septemba 14, 2014
kutakapofanyika mkutano mkuu wake ambako watapata fursa ya kuonyesha
mwendo wa chama hicho.
“Nawashukuru viongozi wangu wakuu bila kujua wamepanga tarehe ya
mkutano huo siku niliyozaliwa, lakini sikubatizwa hadi siku ya Uhuru
Desemba 12, 1961, viongozi wa Chadema wamepanga kufanyika mkutano mkuu
siku ya sherehe ya kuzaliwa kwangu na wale wanaoiombea ajali Chadema
hawatafanikiwa,” alisema.
Julai 2, mwaka huu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia kwa
Naibu Msajili, Sisty Nyahoza, ilitoa taarifa na kusema kuwa Mbowe hana
sifa za kugombea uongozi wa chama hicho, kwa vile Katiba ya chama hicho
ya mwaka 2006 inambana.
Nyahoza alisema Katiba ya Chadema ya mwaka 2004 ilikuwa na kipengele
cha ukomo wa madaraka kilichoeleza kuwa kiongozi aliyeongoza vipindi
viwili vya miaka mitano mitano hawezi kuwania tena nafasi hiyo.
Mvutano huo ulikifanya chama hicho kumlaumu Msajili, Jaji Mutungi, kikidai ofisi yake inatumiwa na wasaliti wa chama hicho.
Julai mosi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika,
alisema Jaji Mutungi hana mamlaka ya kubaini sifa za viongozi wa chama
hicho, bali wenye mamlaka hayo ni wanachama wa chama hicho pekee.
Mnyika alisema mwaka 2006, katiba ya Chadema haikurekebishwa bali
iliundwa upya na kuridhiwa na mkutano mkuu wa chama na kwamba Agosti 13,
2006 ilizinduliwa na nyaraka zote alikabidhiwa Msajili wa Vyama wa
wakati huo, John Tendwa.

No comments:
Post a Comment