Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
BUNGE
Maalum la Katiba leo tarehe 9 Septemba, 2014 limeanza kazi yake ya
kusoma na kujadili taarifa za Kamati mbalimbali zikiwemo Kamati namba
Kumi na Mbili, Kamati namba Mbili, Kamati namba Moja, Kamati namba Nne,
Kamati namba Nane, Kamati namba Tano, Kamati namba Tisa, Kamati namba
Tatu, Kamati namba Sita pamoja na Kamati namba Kumi na Moja.
Baadhi
ya mambo yaliyojadiliwa katika Bunge hilo ni pamoja suala la baadhi ya
viongozi kumiliki akaunti zao za fedha nje ya nchi, haki za makundi
mbalimbali nchini, haki za binadamu, masuala ya ndoa ya jinsia moja,
haki za wafanyakazi na ajira, wajibu wa Waajiri nchini, haki za uzazi
kwa wanawake, haki ya kuishi na sheria ya kunyonga, pia mambo yanayohusu
Muundo wa Baraza la Usalama la Taifa.
Akizungumza
wakati wa mjadala huo katika Bunge hilo, mjumbe wa Kamati namba Sita,
Mhe. Charles Mwijage amesema kuwa si vema kwa viongozi nchini kujenga
tabia ya kufungua akaunti na kuweka fedha zao nje ya nchi kwani
kunakaribisha masuala ya wizi wa fedha toka ndani ya nchi kwenda nje ya
nchi.
“Ni
vema kiongozi yoyote anayetaka kumiliki fedha nje ya nchi aeleze ni
wapi anamiliki hizo akaunti na nini anamiliki”, alisema Mhe. Mwijage.
Naye
Mjumbe wa Kamati namba Tatu, Mhe. Nyambari Chacha Nyangwine amegusia
kuhusiana na suala hilo akisema kuwa kuna haja ya kuwekwa kwa sheria
itakayowabana viongozi wenye tabia ya kufungua akaunti za fedha nje ya
nchi ili hali hiyo isiwepo nchini.
“Mambo
ya kiongozi wa umma kumiliki akaunti ya fedha nje ya nchi si jambo
jema, sheria izuie na ni vema kiongozi yoyote wa umma anayetaka kufanya
hivyo basi afungue akaunti yake ndani ya nchi na sio vinginevyo”,
alisema Nyangwine.
Mhe.
Nyangwine pia amezungumzia kuhusu kuendelezwa kwa sekta ya viwanda
nchini ili kuweza kujikwamua kiuchumi, hivyo ameisisitizia Serikali
kuviendeleza viwanda vyake ili uchumi wa nchi uweze kukua na kuleta
maendeleo kwa wananchi.
Aidha,
alliongeza kuhusu haki za wanaume huku akisema kuwa wanaume tayari wao
wanazo haki zao tangu kuzaliwa kulingana na maandiko ya dini
yanavyosema, hivyo ni vema sasa wanawake wakapewa kipaumbele kwa kupewa
haki sawa yaani hamsini kwa hamsini.

No comments:
Post a Comment