Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma.
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta
amewaadaa baadhi ya viongozi wanaojiita UKAWA kwa taarifa yao ya kutaka
kumfikisha Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa kwa kuendeleza mchakato huo
wa Katiba.
Kauli hiyo imetolewa leo 12 Septemba, 2014 mjini Dodoma na
Mhe. Sitta kufuatia baadhi ya viongozi hao, kudai kuwa watampeleka
katika mahakama hiyo.
Mhe. Sitta ameeleza kuwa baadhi ya viongozi wa kundi hilo
kuwa wanakipaji kikubwa cha uigizaji huku akifafanua kuwa wakati
walipokuwa Bungeni wakati wa mchakato wa kupiga kura za siri, viongozi
wa kundi hilo walizifanya kura hizo kuwa wazi na baadaye kuja na kauli
kuwa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea sasa sio halali lihairishwe.
“Juzi Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekutana nao
mara mbili kwa muda wa saa Saba na katika kukutana huko wakafikia
maafikiano, lakini siku moja baadaye wao wamekana yote waliyokubaliana
hapa mjini Dodoma, kwa hiyo ni vyema wananchi wakawapima hawa watu”,
alisema Mhe. Sitta.
Aidha, Mhe. Sitta aliasa kwa kusema kuwa wananchi na
viongozi wanatakiwa kujua kuwa mchakato wa bunge Maalum la Katiba sio
jambo la mzaha na wao hawapo hapo bungeni kwa mzaha mzaha.
“Mimi nawaambia kuwa hapo mwakani watakaposhindwa uchaguzi
basi warejee katika fani zao ambazo Mwenyezi Mungu kawajalia”, alisema
Mhe. Sitta.

No comments:
Post a Comment