Na Magreth Kinabo, Dodoma
Mjumbe
wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Profesa Mark Mwandosya amependekeza
kwamba suala la rushwa litambuliwe Katiba Mpya, inayopendekezwa ili
kuweza kuongeza nguvu ya kupambana nalo.
Kauli
hiyo imetolewa leo na Mwandosya, ambaye pia Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais (Kazi Maalum) wakati akichangia mjadala wa kujadili sura
zilizobakia za Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kikao cha thelasini na saba
cha Bunge hilo linaloendelea mjini Dodoma, ambacho kinaendelea na sura
ya Pili, Tatu, Nne na Tano za Rasimu hiyo.
Mhe.
Mwandosya alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akichangia sura ya Tatu
kuhusu Maadili ,Miiko ya Uongozi na Utumishi wa Umma.
“ Lazima suala la rushwa litambuliwe katika Katiba hii.Serikali
zote mbili zitatunga sheria ili tuweze sasa kupigana na adui rushwa. Ni
suala la kwetu sote halina muungano, lazima litambuliwe vinginevyo hii
vita tutashindwa,” alisisitiza Mhe. Mwandosya.
Akizungumzia
kuhusu suala la rushwa mjumbe mwingine wa Bunge hilo, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjwela akichangia sura hiyo alisema rushwa ni adui wa haki dunia
nzima na Tanzania inaelewa pia ni sehemu ya utawala bora.
“Hili
ni jambo linalorudisha maendeleo nyuma.Mimi ninawaomba wajumbe wenzangu
tuliingize katika Katiba tusipoliingiza tutakuwa hatueleweki,” alisema
Dkt. Mwanjwela.
Aidha Mhe. Mwandosya alisisitiza katika sura ya pili kupata bidhaa na huduma bora zenye viwango ni jambo muhimu.
Aliongeza kuwa kiuchumi Serikali itachukua hatua zinazofaa… ili kuwezesha ushindani wenye hali ya tija.
“ Regulation liwe kwenye Katiba itakuwa ni mapinduzi… si suala la Serikali bali la vyombo maalum,” alisema.
Profesa
Mwandosya akichangia kuhusu sura ya Nne inayohusu Haki za Binadamu
alisema mazingira safi ni suala mtambuka ni vema kuwa katika Katiba,
kila Mtanzania kupata maji safi na salama, hivyo Katiba inaweza kusema
kwani ni jambo la kitaifa ambalo litafanikiwa kwa kuwa ni wajibu wa
Serikali , lakini si kwa kuipeleka mahakamani.
Alizungumzia
pia kuhusu nyumba na makazi bora ni haki ya binadamu inaendana na
mazingira safi na salama, hivyo likiwekwa katika Katiba ni lazima kila
Mtanzania ataishi katika mazingira safi na salama.

No comments:
Post a Comment